Mabikira 'watakatifu' wanaoolewa na Yesu
Jessica Hayes alijinunulia mwenyewe shela, ushungi na pete ya ndoa. Lakini aliposimama altareni kufungishwa ndoa na Askofu, hakuwepo bwana harusi pembeni yake. Alikuwa akifunga ndoa na Yesu Kristo.
Bi Hayes, 41, ni mwanamke bikra aliyejihifadhi ili awe mke wa Mungu. Hii ni ada ambayo si ya lazima wanayoweza kufanya wanawake wanaoamini katika ukatoliki kwa kujitoa wakfu miili yao kwa Bwana kwa maisha yao yote.
Lakini hata ndani ya Ukatoliki, ada hii inayofahamika kwa kingereza kama consecrated virgins si maarufu- na waumini wachache wanafahamu juu ya mabikra hao- moja ya sababu ni kuwa ada hiyo iliruhusiwa kwa uwazi na kanisa chini ya miaka 50 iliyopita.
Katika sherehe ya wakfu ama harusi, mwanamke bikra ambaye huvaa shela jeupe- hula kiapo cha maisha cha kutojihusisha na mahusiano ya kimapenzi na kutokufanya ngono.
Wanawake hao pia huvaa pete za ndoa - ambayo huwa ni alama ya kufunga uchumba ama ndoa na Kristo.
"Mara nyingi naulizwa: 'Kwa hiyo, umeolewa?'" anasema bi Hayes. "Kawaida huwajibu kuwa mimi ni sawa tu na wanawake watawa (masista) wa kanisa, na nimejitoa kwa Kristo kwa moyo wote, tofauti mie naishi nje na watu wa kawaida.
Mwanamke huyo ni mmoja kati ya "wake wa Kristo" 254 wanaoishi nchini Marekani kwa mujibu wa taasisi yao iitwayo United States Association of Consecrated Virgins (USACV). Wanawake hao wanafanya kazi mbali mbali ikiwemo zima moto, uhasibu, ualimu na wengine ni wafanyabiashara.
Duniani kote kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2015 kuna wanawake kama hao 4,000 huku Vatican (makao makuu ya kanisa katoliki) ikisema ada hiyo imekuwa ikipata wafuasi wengi katika miaka ya karibuni kutoka maeneo tofauti ya dunia.
Tofauti na masista, mabikra watakatifu ama wake wa Yesu, hawaishi kwenye makao maalumu ya kanisa ama kuvaa nguo maaalumu; wanaishi maisha ya kawaida, wanafanya kazi na wanijetegemea kwenye kuendesha maisha yao ya kila siku.
Hakuna ada kama hiyo kwa wanaume ndani ya Kanisa Katoliki. Ufaransa na Italia wanaongoza kwa kuwa na mabikra watakatifu 1200 kwa ujumla. Nchi nyengine kama Mexico, Romania, Poland, Uhispania, Ujerumani, Argentina na Marekani pia zina wanawake kama hao wengi.
Kufikikia mwaka 2020 idadi ya wake wa Kristo inatarajiwa kufikia 5,000. "Mimi ni mwalimu kwa miaka 18 sasa na ninafundisha shule ya sekondari ambayo pia nilisoma," anasema Bi Hayes, ambaye ni mkaazi wa Fort Wayne, jimboni Indiana, Marekani.
"[Kabla ya wakfu] Niligundua kuwa sikuwa na wito wa kuhudumia na kuishi katika jamii kama wafanyavyo masista, iwe katika mkusanyiko wa kanisa ama mashirika ya kiutume."
Anapokuwa hayupo shuleni bi Hayes anatumia muda wake mwingi kufanya ibada na toba. Pia huripoti kwa Askofu na mshauri wake wa masuala ya kiroho.
"Naishi na jamii ya watu, nipo chini ya parokia ambayo ipo maili mbili kutoka ninapoishi. Nipo tayari muda wote kuwasaidia rafiki zangu na ndugu. Na pia nafundisha lakini juu ya yote hayo napata wakati mtakatifu kwa ajili ya Bwana."
Anasema alishawahi kuwa katika mahusiano ya kimapenzi (bila kufanya ngono) lakini mahusiano hayo hayakumtosheleza. "Nilihisi wito wa kuolewa, na hilo ni jambo la asili kwa wanaadamu. Hivyo, nikaingia kwenye mahusiano...lakini sikuwa na yakini."
Wanawake bikra wamekuwa sehemu ya kanisa toka miaka ya mwanzo ya Ukristo. Katika karne tatu za mwanzo baada ya kristo (AD), wengi waliuawa kama mashahidi.
Miongoni mwa hao ni Agnesi wa Roma (Agnes of Rome) ambaye anaripotiwa kuuawa kutokana na kujitoa kwake kwenye usafi wa kidini.
Hata hivyo ada hiyo ilififia katika zama hizo za kale ambapo maisha ya utawa yalishamiri. Mwaka 1971 chapisho la kanisa liitwalo Ordo consecrationis virginum, lilihuisha utaratibu huo wa kujitolea.
Bi Hayes anasema alianza kufikiria maisha yake ya sasa baada ya kukutana na mshauri wake wa maswala ya kiroho, ambaye, "alianza kuniuliza mawali sahihi"
Aliamua kuishi kama bikra mtakatifu mwaka 2013, na akatiwa wakfu (kuolewa) miaka miwili baadae akiwa na miaka 36.
"Japo nilikuwa na majukumu saswa tu na kabla ya wakfu, sasa hivi mahusiano na Bwana ni tofauti kwa sababu ni mwenza wangu na si rafiki."
Kuishi katika jamii ambayo mahusiano ya kimapenzi yanapewa umuhimu mkubwa ni changamoto kubwa kwa mabikra hao amabo hufumbia macho mahusiano ya kimwili kwa maisha yao yote.
"Jambo gumu zaidi naamini ni kutokueleweka, wengi wanaona tufanyacho ni kwenda kiyume na utamaduni," anasema bi Hayes.
"Wengi huniuliza 'Oh, kwa hiyo wewe ni kama mtu asiye na mpenzi.' Inanipasa niwaambie kuwa Bwana ndiye mwenza wangu, na kuwa nimempa mwili wangu yeye."
Je, ni kweli hawajaingiliwa kimwili?
Mwezi Julai kanuni mpya zilichapishwa na Vatcan kuhusu ada hiyo, na baadhi ya mabikra watakatifu hawakuzifurahia.
Swali kubwa lilikuwa iwapo wanawake wanaotaka kuishi katika wito huo lazima wawe bikira hata kabla ya kuwekwa wakfu au kuishi maisha ya kujitunza baada ya kuwekwa wakfu.
Tofauti na watawa (masista) ambao maisha ya kutojihusisha na mahusiano ya kimapenzi huanza tu mara baada ya kula kiapo. Wake wa Yesu kwa mujibu wa tamaduni wanatakiwa wawe mabikira haswa.
Katika kifungu cha 88 cha kanuni hizo, Vatican ilisema; "kuutunza mwili wake na kutojihusisha na ngono ni jambo jema sana, ni kitu muhimi lakini si cha lazima (ili mwanamke awe Mke wa Yesu)." Kwa lugha nyepesi si lazima mwanamke awe hajaingiliwa ili awe Mke wa Yesu.
Hata hivyo taasisi ya USACV, ambayo bi Hayes ni mwanachama wamesikitishwa na kanuni hizo. Katika tarifa yao, USACV wamesema "wameshtushwa kusikia Kanisa Kuu linasema ubikra inaweza isiwe sifa ya kupatiwa wakfu wa kuwa mke wa Bwana."
Bi Hayes anatamani kama kungekuwa na maelezo ya zaidi na ya wazi kuhusu kanuni hizo mpya, lakini anafurahi kuona Papa ameweka msisitizo zaidi kwenye wito.
"Chapisho pia linasema anayetaka kuwa Mke wa Yesu hatakiwi kuwa ni mtu amabaye alishaolewa kabla ama kuvunja usafi wake kwa kujihusisha na ngono hadharani," amesema.
"Labda kuna tukio ambalo ulilifanya huko nyuma ukiwa na umri mdogo, ama mwanamke alibakwa na hivyo sio bikira kwa sababu ya utashi wake," amesema bi Hayes akitafakari kwanini Papa amefanya mabailiko hayo ya kikanuni. Mwishowe anaamini, kanuni hizo zinalenga kuwahamasisha wanawake wa kikatoliki kujitoa zaidi na kukumbatia wito huo.








No comments