Kaka ya Floyd kuhutubia mdahalo wa UN kuhusu ubaguzi wa rangi Marekani
Kaka yake George Floyd, Mmarekani mweusi ambaye kifo chake kilitokea akiwa mikononi mwa polisi weupe na kuzusha maandamano makubwa ya kupinga ubaguzi, ameuomba Umoja wa Mataifa uunde tume huru ya kuchunguza mauaji ya Wamarekani wa asili ya Afrika yanayofanywa na polisi.
Kaka yake Floyd, Philonise ameyasema hayo wakati akihutubia Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binaadamu lililoandaa mdahalo wa dharura jana kujadili "ubaguzi wa rangi wa kimfumo" nchini Marekani na kwingineko.
Nchi za Kiafrika zinamshinikiza Kamishna wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet, kuchunguza ubaguzi wa rangi na ukiukaji wa uhuru wa raia unaofanywa na polisi dhidi ya watu wa asili ya Kiafrika nchini Marekani.
Akiuhutubia mkutano huo, Bachelet ametoa wito kwa nchi kupambana na matukio ya zamani ya utumwa na ukoloni na kutoa fidia. Wiki iliyopita, aliliomba Bunge la Marekani kupitisha mageuzi ambayo yatawawajibisha polisi kwa ukatili wao. Hapo jana, Rais Donald Trump alisaini amri ambayo amesema itahimiza utendaji kazi mzuri wa polisi.
No comments