Breaking News

Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte asema Mungu ni 'mpumbavu'

Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte amemwita Mungu "mpumbavu", hatua ambayo imekera sana watu katika taifa hilo lenye Wakatoliki wengi.
Kiongozi huyo amesema hayo kwenye hotuba iliyopeperushwa moja kwa moja kupitia runinga.
Aidha, amekosoa vikali hadithi ya Adam na Hawa kuhusu jinsi walivyotenda dhambi na kuondolewa kutoka kwenye neema ya Mungu.
Kadhalika, amekosoa wazo kwamba kila binadamu tangu wakati huo huzaliwa akiwa na dhambi asilia.
Bw Duterte anajulikana sana kwa matamko yake yenye kuzua utata pamoja na matusi yenye kutumia lugha kali dhidi ya wapinzani wake.
Ingawa kanisa na raia wamemshutumu kwa hilo, ofisi ya rais huyo imesema alikuwa tu anaeleza imani yake binafsi.
Rais huyo amewahi kumshutumu pia Papa kwa kutumia maneno makali na ana historia pia ya kuwatusi viongozi wengine.
Tamko la sasa alilitoa katika hotuba mji wa Davao, mji ambao alikuwa kiongozi wake kabla ya kuwania urais.
Huku akiuliza "Ni Mungu yupi huyu mpumbavu?", Bw Duterte amekosoa hadithi ya Biblia kuhusu kuumbwa kwa dunia na binadamu na kufukuzwa kwa Adam na Hawa kutoka Shamba la Eden baada ya kula "tunda walilokatazwa".
"Uliumba kitu kisicho na doa na kisha ukafikiria tukio la kuweka uumbaji wako kwenye vishawishi na kuharibu ubora wa kazi yako," amesema.
Askofu wa kanisa Katoliki eneo hilo Arturo Bastes amejibu kwa kumweleza rais huyo kama "mwenda wazimu" na kutoa wito kwa watu kumuombea kwa sababu ya "maneno yake ya kufuru na tabia za kidikteta."

No comments