Hosni Mubarak: Aliyekuwa rais wa Misri, afariki akiwa na umri wa miaka 91
Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak afariki dunia hospitalini jijini Cairo akiwa na miaka 91.
Mubarak alidumu madarakani kwa miongo mitatu kabla ya kung'atuliwa jeshi baada ya maandamano makubwa ya raia.
Alikutwa na hatia ya kula njama katika mauaji ya waandamanaji wakati wa mapinduzi na kuwekwa kizuizini.
Hata hivyo, hatia hiyo iliondolewa na akaachiwa huru mwezi Machi 2017.
Kifo chake kimethibitishwa na Televisheni ya taifa ya Misri leo Jumanne. Mapema tovuti ya Al-Watan iliripoti kuwa kiongozi huyo alifariki kwenye hospitali moja ya jeshi.
Mubarak alifanyiwa upasuaji mwishoni mwa mwezi Januari.
Je, Mubarak alikuwa nani?
Baada ya kuzaliwa mwaka 1928, Mubarak aliingia jeshi kama kijana na kuendelea kuchukua jukumu muhimu katika vita kati ya Israel na Waarabu 1973.
Alikuwa rais chini ya muongo mmoja baadaye , kufuatia ,mauaji ya rais Anwar Sadat.
Alikuwa na jukumu muhimu katika mchakato wa amani wa Israel - Palestina
Lakini licha ya mabilioni ya madola ya misaada ya kijeshi ambayo Misri ilipokea wakati alipokuwa madarakani , ukosefu wa ajira, ufukara, na ufisadi uliendelea kuimarika.
Mwaka mmoja baada ya Mubarak kupinduliwa, Mohammed Morsi mwanasiasa Muislamu , alishinda uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini Misri .
Morsi yeye mwenyewe alitimuliwa madarakani na jeshi 2013 na kufariki 2019 akiwa jela.
Mubarak, wakati huohuo, alifungwa kifungo cha maisha kufuatia vifo vya waandamanaji 900 ambao waliuawa na vikosi vya usalama wakati wa maandamano ya 2011.
Mashtaka hayo baadaye yalifutiliwa mbali na Mubaraka kuachiliwa 2017
Mgogoro ulizuka mnamo mwezi Januari 2011, baada ya maandamano kama hayo kutokea Tuinisia na kusaidia kupinduliwa kwa rais wa taifa hilo.
Mubarak alilazimishwa kujiuzulu siku 18 baadaye.
No comments