Breaking News

Vifo vya corona Iran vyapindukia 9,000, Ujerumani yazinduwa 'app' ya kufuatilia maambukizo

Serikali ya Ujerumani imesema kwamba haitakuwa lazima kwa watu kutumia programu maalum ya kufuatilia maambukizo ya korona kupitia simu zao. Msemaji wa serikali, Steffen Seibert, alisema hapo jana kwamba hakuna atakayeadhibiwa kwa kutokutumia programu hiyo wala kuzawadiwa kwa anayetumia.

Programu hiyo iliyopewa jina la Corona-Warn-App imeanza kazi leo, ikidhamiriwa kuwapa watu indhari juu ya maambukizo ya korona na pia kuwasaidia kupata taarifa kuhusu hali zao binafsi. Hayo yakijiri, Iran imesema kuwa watu waliokufa kwa virusi vya korona nchini humo imepindukia 9,000 baada ya kuripoti vifo 100 kwa siku tatu mfululizo.

Msemaji wa wizara ya afya, Sima Sadat Lari ameonya kwamba kuongezeka harakati za kusafiri miongoni mwa raia kumechochea maambukizo kusambaa, huku akisema kwamba hali huenda ikawa mbaya zaidi. Kufikia jana, taifa hilo la Ghuba ya Uajemi lilikuwa limesajili watu 192,439 walioambukizwa maradhi hayo ya COVID-19, ingawa wakosoaji wake wengi wanasema huenda idadi ni kubwa zaidi ya hapo.

No comments