Kombe la Dunia 2018: Mo Salah ana matumaini ya kucheza asilimia zote
Kocha wa timu ya taifa ya Misri Hector Cuper amesema kuna uwezekano wa "karibu 100%" kuwa mshambuliaji Mohamed Salah atacheza mechi yao ya kwanza Kombe la Dunia mwaka huu leo Ijumaa dhidi ya Uruguay.
Mechi hiyo itachezewa mjini Yekaterinburg na itaanza saa tisa alasiri saa za Afrika Mashariki.
Salah, 25, hajacheza tangu alipoumia begani wakati wa fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Ulaya mnamo 26 ambapo timu yake ya Liverpool ilishindwa 3-1 na Real Madrid.
"Ninaweza kuwahakikishia karibu 100% kwamba atacheza, pengine kutokee mambo yasiyotarajiwa dakika za mwisho," amesema Cuper.
Cuper amesema Salah "anafanya vyema sana" na kwamba alipata nafuu "haraka sana, sana."
Aliongeza: "Tunajaribu kumfanya ajiamini zaidi. Madaktari wanampa fursa ya kuamua kama atacheza au hatacheza, lakini namfahamu Salah vyema sana na nina uhakika kwamba hana wasiwasi, hana woga."
Beki wao Ali Gabr pia anatarajiwa kuwa sawa kucheza baada ya kuumia usoni wakati wa mazoezi.
Uruguay upande wao wanatarajiwa kuchezesha kikosi cha wachezaji wachanga hasa safu ya kati, ambapo watakuwa pia na kiungo wa kati wa miaka 20 Rodrigo Bentancur na Nahitan Nandez, 22.
Lakini kwingineko, kikosi chao kina wachezaji wazoefu, na hata zaidi safu ya mashambulizi ambapo wana Luis Suarez na Edinson Cavani. Mataifa hayo mawili yamo Kundi A pamoja na Urusi na Saudi Arabia.
Madaktari wa timu walisema baadaye kwamba wanafuatilia hali yake siku baada ya siku. Cuper alipuuzilia mbali umuhimu wa mchezaji huyo na kusema "mbinu zetu hazimzunguki mchezaji huyo pekee."
Kuangaziwa zaidi kwa nyota huyo wa Liverpool huenda kukawasaidia Uruguay, ambao wamekuwa hawaangaziwi sana licha ya kuwa wanapigiwa upatu kushinda Kundi A.
Wana kikosi chenye wachezaji wazoefu sana, ambapo wachezaji wanne wao wamecheza zaidi ya mechi 100 za kimataifa, na kipa wao Fernando Muslera (97) na mshambuliaji Luis Suarez (98) wanatarajiwa kucheza mechi mia wakifikia hatua ya kumaliza hatua ya makundi.
Washambuliaji wao wawili Suarez na Edinson Cavani wamefunga zaidi ya mabao 93 mechi ya kimataifa kwa pamoja.
Wengi wanatarajia Uruguay washinde. Wanaelekea kwa mechi hiyo wakiwa wameshinda mechi tatu mtawalia. Misri hawajashinda mechi hata moja 2018 na bado hawajashinda mechi yoyote Kombe la Dunia.
No comments