Kroos ayafufua matumaini ya Ujerumani
Kiungo wa kati wa Ujerumani Toni Kroos alifunga goli katika dakika ya tano ya muda wa ziada na kuwapa Ujerumani ushindi wa 2-1 walipokuwa wakicheza na Sweden katika mechi yao ya pili ya Kundi F kwenye Kombe la Dunia.
Ujerumani walikuwa wanahitaji angalau sare kwenye mechi hiyo ili wayaweke hai matumaini yao ya kufuzu kwenye hatua ya mtoano baada ya kulazwa na Mexico kwenye mechi ya kwanza.
Kroos ambaye ameshambuliwa na wachambuzi kwa kutoiongoza Ujerumani baada ya kustaafu kwa Bastian Schweinsteiger na Philip Lahm, alijitokeza katika hizo sekunde za mwisho za mechi ili apige mkwaju wa frikiki ambao walipewa Ujerumani baada ya Timo Werner kuangushwa upande wa kushoto nje ya eneo la hatari.
Huku mechi ikiwa sare ya 1-1 Kroos alimuanzia pasi fupi Marco Reus ambaye alimsimamishia mpira na kumpa nafasi ya kuipiga frikiki hiyo kwa utaalam na kuwapa goli la ushindi mabingwa hao watetezi wa dunia.
Ujerumani walikuwa wanacheza na wachezaji kumi uwanjani baada ya Jerome Boateng kuondolewa uwanjani alipoonyeshwa kadi ya pili ya njano kwenye dakika ya 82 ya mechi alipomchezea vibaya mshambuliaji wa Sweden Marcus Berg. Mapema kwenye kipindi hicho cha pili Boateng alikuwa ameonyeshwa kadi ya kwanza ya njano.
Iwapo Ujerumani wangeshindwa mechi hii ingemaanisha kwamba wameondolewa mapema kwenye hatua ya makundi katika Kombe la Dunia na ni jambo ambalo lingekuwa limefanyika kwa mara ya kwanza kwa taifa hilo lenye ufuasi mkubwa wa mchezo wa mpira tangu mwaka 1938.
No comments