Rais Emmerson Mnangagwa anusurika kuuawa mjini Bulawayo
Taarifa kutoka nchini Zimbabwe zinasema Rais Emmerson Mnangagwa amenusurika kuuawa, baada ya mripuko kutokea katika uwanja ambako alikuwa akifanya mkutano wa kampeni.
Mripuko huo ulitokea wakati Mnangagwa akiwapungia mkono wafuasi wake kwenye mkutano wa kampeni katika mji wa pili kwa ukubwa, Bulawayo, kuelekea uchaguzi mkuu wa hapo mwezi ujao.
Msemaji wake, George Charamba, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba rais huyo mwenye umri wa miaka 75, ambaye kwenye mkutano huo alikuwa ameambatana na makamu wake wawili, yuko salama kwenye ikulu ndogo mjini humo.
Hata hivyo, makamu wote wawili wa rais, Constantino Chimwanga na Kembo Mohadi wamejeruhiwa, sambamba na maafisa kadhaa wa chama tawala cha ZANU-PF.
Tukio hilo limetokea mnamo ambapo Umoja wa Ulaya ukianza kusambaza waangalizi wa uchaguzi nchini Zimbabwe, kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 16 kuelekea uchaguzi wa mwezi ujao. Uchaguzi huo utakaofanyika Julai 30 utakuwa wa kwanza katika nchi hiyo tangu, kiongozi mkongwe Robert Mugabe alipoondolewa kufuatia mapinduzi ya kijeshi mwezi Novemba baada ya kuwepo madarakani kwa miaka 37.
No comments