Breaking News

Staa wa zamani wa liverpool hyypia ajitosa kuwawezesha wachezaji wa Tanzania


Gwiji la soka la klabu kongwe barani Ulaya ya Liverpool, Sami Hyypia amesema wachezaji wa Tanzania na Afrika kwa ujumla wana fursa ya kucheza soka la kulipwa nchini Uingereza na nyingine endapo wataongeza bidii.

Hyypia ambaye Jumamosi atazindua mashindano ya Standard Chartered Cup pamoja na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwenye viwanja vya Dar es Salaam Gymkhana amesema kuwa kwa sasa kuna wachezaji wengi wenye vipaji ambao wanatamba Uingereza kwa sababu ya bidii.

Amesema toka enzi ya Tony Yeboah ambaye alicheza naye, kuna wachezaji wengine kama Sadio Mane, Mohamed Salah na wengine wengi wanaotamba katika ligi mbalimbali barani Ulaya na kwingine.

Bila kuwataja majina wachezaji hao, Ligi Kuu ya Tanzania inaaminika kuwa na wenye vipaji kama Ibrahim Ajib wa Yanga na Shiza Kichuya wa Simba.

Amesisitiza, atafanya mazungumzo na Shirikisho la Kandanda Nchini (TFF) kupitia benki ya Standard Chartered ili kuona wanafanya jitihada gani ili kuwawezesha wachezaji wa Tanzania kucheza soka nchini Uiengereza na nchi nyingine kama Finland.

“Kwa sasa nipo Tanzania na bahati nimekutana na viongozi wa TFF hasa kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi, pia nitakutana na Waziri wa Michezo, nini kitafanyika, naomba msubiri,” alisema Hyypia.
Awali, Mkurugenzi wa benki ya Standard Chartered, Sanjay Rughani alisema kuwa wamefarijika kwa ujio wa Hyypia na mbali ya kuzindua mashindano Standard Chartered Cup Jumamosi, pia atakutana na watoto mbalimbali ambao wazazi wao wana akaunti kwenye benki yao na pia mashabiki wa timu wa Liverpool.

Rughani alisema kuwa Hyypia pia atakutana na wachezaji 224 kutoka timu 32 zitakazoshiriki katika mashindano ya mwaka huu ambapo mshindi atapata fursa ya kwenda Liverpool, mwezi Septemba.

“Maandalizi yamekamilika na timu zote zipo tayari kwa mashindano, ili kuonyesha kuwa tupo katika jamii, Hyypia pia atakutana na watoto yatima na kushiriki nao katika shughuli maalum,” alisema Rughani.

No comments