Breaking News

Trump asema Korea kaskazini bado ni 'tishio kubwa'

Rais wa Marekani Donald Trump ameidhinisha upya vikwazo dhidi ya Korea kaskazini akitaja taifa hilo kuwa 'tishio liliso la kawaida' kutokana na silaha zake za nyuklia - siku 10 tu baada ya kutamka kwamba hakuna hatari yoyote kutoka kwa Pyongyang.
"Hakuna tena tishio kutoka Korea kaskazini," alituma ujumbe mnamo Juni 13, siku moja baada ya kukutana na kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong-un huko Singapore.
Hatua hiyo imekuja wakati Marekani na Korea kusini zimefutilia mbali mazoezi mawili ya pamoja ya kijeshi.
Wizara ya ulinzi Marekani Pentagon imesema lengo ni kuunga mkono majadiliano ya kidiplomasia.
Inafuata uamuzi wa mapema wiki hii kusitisha mazoezi makubwa ya kijeshi ya pamoja katiya Marekani na Korea kusini yaliopangwa Agosti.
Rais Trump ameahidi kusitisha 'uchokozi wa kivita' wa kila mwaka kati ya washirika katika hatua ambayohaikutarajiwa kwenye mkutano wake na Kim, akiutaja kuwa "uchokozi" na "ulio na gharama kubwa".
Hilo limezusha mshtuko kwa wengi, kutokana na kuwa katika siku za nyuma Marekani imelalamika kuwa mazoezi hayo ni ya ulinzi tu na yalio muhimu kwa muungano wake wa kijeshi na Seoul.
Katika mkutano huo wa kihistoria kati ya rais wa sasa wa Marekani na kiongozi wa Korea kaskazini Viongozi hao walisaini taarifa ambapo Marekani iliahidi usalama kwa KOrea kaskazini na mwenzake akaahidi "kushughulika kusitisha mipango ya nyuklia katika rasi ya Korea" - pasi kufafanua maana ya ndani ya makubaliano hayo.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amesema kuwa vikwazo dhidi ya Korea kaskazini vitasalia wakati majadiliano yanaendelea kuhusu silaha zake za nyuklia.
Hatahivyo, vyombo vya habari Korea kaskazini vimeripoti kuwa Trump alikubali 'kuondosha vikwazo' wakati uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ukiendelea.

No comments