Sudan Kusini yasema imemchoka kiongozi wa waasi Machar
Serikali ya Sudan Kusini imetangaza leo kuwa imechoshwa na kiongozi wa upinzani Riek Machar, hatua ambayo ni pigo kwa juhudi za karibuni za kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya miaka minne.
Matumaini ya kupatikana suluhisho yaliongezeka wiki hii baada ya Ethiopia kusimamia mazungumzo ya ana kwa ana kwa mara ya kwanza katika miaka miwili kati ya Machar na mpinzani wake mkali Rais Salva Kiir.
Viongozi wa kikanda pia walikuwa Addis Ababa ili kusuruhisha mgogoro huo. Lakini akizungumza leo, siku moja baada ya mkutano huo wa kilele, msemaji wa serikali ya Sudan Kusini, Michael
Makuei, alisema watu wa Sudan Kusini, wakiongozwa na rais wao, wamemchoka Machar. Makuei alikataa uwepo wa Machar katika serikali yoyote ya mpito, lakini hakufuta uwezekano wa kushirikishwa kwa viongozi wengine wa waasi.
Kundi la Machar la SPLM-IO limelaani matamshi ya Makuei likisema yanalenga kuhujumu mchakato wa amani.
No comments