Breaking News

Mkuu wa polisi wa Atlanta ajiuzulu baada ya Mmarekani mwingine mweusi kuuawa


Mkuu wa polisi wa Atlanta nchini Marekani amejiuzulu jana Jumamosi ikiwa ni saa chache baada ya Mmarekani mwingine mweusi kuuawa, kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi wakati walipokuwa wakijaribu kumfanyia kipimo cha kubaini ikiwa ametumia kilevi. Maafisa hao walisema mwanaume huyo alikwapua bastola ya kutia ganzi kutoka kwa polisi mmoja na alipigwa risasi wakati alipokuwa akikimbia. Mauaji ya Rayshard Brooks aliyekuwa na umri wa miaka 27 yamechochea wimbi jipya la maandamano mjini Atlanta, baada ya wimbi la maandamano yaliyofuatia kifo cha George Floyd mjini Minneapolis. Meya wa Atlanta Keisha Lance Bottoms alitangaza kujiuzulu kwa mkuu wa polisi jana Jumamosi wakati watu wapatao 150 walipoandamana nje ya mgahawa wa Wendy ambako kijana huyo aliuawa Ijumaa jioni. Pia alitangaza kufutwa kazi kwa afisa wa polisi aliyefyatua risasi.

No comments