Maelfu wakimbia kusini mwa Syria kwa kuhofia vita
Takribani watu 12,500 wameyahama makaazi yao katika mkoa wa kusini mwa Syria wa Daraa katika muda wa saa 48 zilizopita, wakihofia vita vinavyotarajiwa kati ya vikosi vya serikali na washirika wao dhidi ya wapiganaji wa upinzani kuwania udhibiti wa eneo hilo.
Mkuu wa shirika la uangalizi wa haki za binadamu la Syria Rami Abdel-Rahman, amesema watu waliokimbia walikuwa ni kutoka maeneo ya mashariki na kaskazini-mashariki mwa Daraa, ambao ulishuhudia mashambulizi makubwa na mapambano kati ya wanajeshi wa serikali na wapiganaji wa upinzani.
Shirika hilo limesema wapiganaji sita waliuawa katika mapigano hayo, na raia wanane pia waliuawa katika maeneo ya mashariki na kaskazini-mashariki mwa Daraa. Mwanaharakati kutoka Daraa aliejitambulisha kwa jina moja la Iyad, amesema wanawake wengi, watoto na wazee wameondoka katika eneo hilo katika muda wa siku mbili zilizopita.
Rais wa Syria Bashar Al-Assad ameapa kurejesha maeneo yote yanayoshikiliwa na upinzani karibu na mpaka wa nchi hiyo na Jordan, na pia milima ya Golan inayodhibitiwa na Israel. Lakini kamanda wa waasi mkoani Daraa anaetumia jina la Abu Abed al-Joulani, amesema vita hivyo havitakuwa rahisi kwa wanajeshi wa serikali.
No comments