Breaking News

Merkel aahidi mkopo wa dola milioni 100 kwa Jordan

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ameahidi kuipa Jordan mkopo wa dola milioni 100 kuiwezesha nchi hiyo ya kifalme, kutekeleza mageuzi yanayohitajika na Shirika la Fedha Duniani IMF. 

Merkel ametoa ahadi hiyo mjini Amman katika ziara yake ya siku mbili, akisema mkopo huo ni nyongeza kwa ahadi nyingine ya euro milioni 384, ambayo Ujerumani iliahidi mwaka huu. 

Uchumi wa Jordan umeathirika katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na migogoro katika nchi jirani, na ongezeko la idadi ya wakimbizi, hali ambayo iliilazimisha serikali hiyo kuchukua mkopo wa miaka mitatu wa kiwango cha dola milioni 723 kutoka kwa IMF. 

Katika kukabiliana na hali hiyo, serikali ya Jordan ilianzisha hatua kadhaa za kubana matumizi ambazo zilihusisha rasimu ya sheria mpya ya kodi. Hata hivyo mswada huo ulisababisha maandamano ya wiki mzima nchini kote na kulazimisha serikali kujiuzulu. 

Merkel anazuru Jordan na Lebanon huku kipaumbele cha ziara yake kikiwa ni kutafuta suluhisho kwa suala la wakimbizi.

No comments