Viongozi wa kanda wafufua mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini
Waasi wa Sudan Kusini wamesema leo kuwa muda zaidi unahitajika ili kufanikisha upatikanaji wa amani ya kudumu nchini Sudan Kusini, na kwamba itakuwa bora kushughulikia mizizi ya vyanzo vya vita hivyo, vya wenyewe kwa wenyewe.
Kundi hilo la waasi limesema katika taarifa kuwa hakuna njia ya mkato ya kufikia amani, kufuatia mazungumzo kati ya Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi ambaye ni makamu wa zamani wa rais Riek Machar nchini Ethiopia.
Viongozi wa Afrika Mashariki wako mjini Addis Ababa Ethiopia wakitumai kuyafufua mazungumzo ya amani yaliokwama, kufuatia mkutano wa ana kwa ana uliosubiriwa kwa muda mrefu kati ya mahasimu hao.
Kiir na Machar walianza mazungumzo jana wakiongozwa na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, hayo yakiwa mazungumzo yao ya kwanza kwa muda wa karibu miaka miwili.
Yaliyojadiliwa yamesalia kuwa siri, lakini video ya mwanzo wa mkutano wao ilionesha waziri mkuu Abiy akiwa katikati ya viongozi hao hasimu baada ya kuwakumbatia.
No comments