Viongozi wa Ulaya wakutana kujadili suluhisho la mzozo wa wahamiaji
Viongozi wa nchi 16 za Umoja wa Ulaya wanakutana leo mjini Brussels kujadili suluhisho la mzozo wa wahamiaji, ambao umedhihirisha mgawanyiko mkubwa miongoni mwa nchi wanachama wa umoja huo.
Mazungumzo katika mkutano huo yanafanyika siku chache kabla ya mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi zote za umoja huo utakaofanyika Alhamis na Ijumaa.
Mizozo ya hivi karibuni nchini Italia na Ujerumani imerejesha mjadala mkali kuhusu sera ya wahamiaji ya Umoja wa Ulaya, ambao uliibuka wakati wa mgogoro mkubwa wa wakimbizi mwaka 2015.
Nchini Italia, serikali mpya iliizuia meli ya wahamiaji kutia nanga kwenye bandari zake, kama ujumbe kwa nchi nyingine za Ulaya kwamba haitawapokea wahamiaji zaidi.
Nchini Ujerumani Kansela Angela Merkel anakabiliwa na changamoto kutoka kwa waziri wa mambo ya ndani, ambaye anataka kuifunga mipaka ya nchi kwa wahamiaji wapya.
No comments