Ripoti yaelezea mateso wanayopitia Warohingya mikononi mwa serikali

Shirika moja la haki za binadamu limesema kuwa jeshi la Myanmar lilipanga na kutekeleza ukandamizaji mkubwa dhidi ya jamii ya Waislamu wa Rohingya, katika ripoti mpya yenye ushahidi tosha ambao linasema unathibitisha haja ya kufanywa uchunguzi wa mauaji ya halaiki. 


Zaidi ya Warohingya laki saba walikimbilia Bangladesh, ambako walisimulia visa vya kubakwa pamoja na mauaji. 

Shirika la kuteteta haki za binadamu la Fortify, katika ripoti yake iliotokana na uchunguzi wa miezi kadhaa nchini Myanmar na Bangladesh na mahojiano na mamia ya waathirika pamoja na maafisa wa serikali, limegundua kuwa vikosi vya usalama viliwaondolea Warohingya uwezo wa kujilinda kwa kuwanyanganya zana zote za ncha kali, na kutoa mafunzo kwa jamii zisizo za Rohingya kupigana. 

Wakati huo huo, wachunguzi wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa wakimbizi wa jamii ya Waislamu wa Rohingya wanaowasili Bangladesh wasema machafuko, yakiwemo mateso yanaendelea kufanywa dhidi yao nchini Myanmar na kuwa mazingira ya jumla bado ni hatari kwa makundi ya wachache ya kikabila na kidini.

No comments